Wizara ya Mambo ya Ndani ya Syria ilitangaza siku ya Alkhamisi kwamba, gari moja iliyokuwa imeshehenezwa mabomu iliripuka katika eneo la Haram ya Bibi Zainab SA katika viunga vya mji mkuu Damascus. Huo ulikuwa mripuko wa pili kwenye kipindi cha siku mbili dhidi ya Waislamu waliokuwa kwenye maombolezo ya Imam Husain AS ya Tasua na Ashura. Siku ya Jumanne pia, pikipiki moja iliyokuwa imetegwa mabomu iliripuka karibu na basi moja lililokuwa limeegeshwa karibu na Haram ya Bibi Zainab al Kubra SA na kusababisha hasara kwenye eneo hilo pamoja na kujeruhi watu wawili.
Hapa tunaweza kugusia nukta kadhaa kuhusu sababu za kutokea miripuko hiyo ya mfululizo wakati huu wa maomboleza ya Muharram, katika Haram ya Bibi Zainab al Kubra SA huko Damascus Syria.Mosi: Miripuko imetokea huko Damascus katika siku 10 za mwanzo za mwezi huu wa Muharram, wakati Waislamu wakiwa kwenye maombolezo ya Imam Husain AS. Tena magaidi walichagua siku kama za Tasua na Ashura kufanya jinai yao hiyo. Duru za habari zimeripoti kuwa, mripuko mmoja ulitokea wakati Waislamu wakigawa chakula cha nadhiri kwa waombolezaji. Aidha miripuko hiyo kwenya Haram ya Bibi Zainab SA mjini Damascus Syria imetokea sambamba na kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Ulaya Magharibi za Sweden na Denmark. Ni kwa sababu hiyo ndio maana wachambuzi wa mambo wakasema kuwa, lengo la magaidi hao ni kuendeleza mtindo ule ule wa kupinga dini unaoshuhudiwa katika nchi za Magharibi. Pili: Miripuko ya kigaidi nchini Syria imekwenda sambamba na mashambulio ya utawala wa Kizayuni dhidi ya ya Syria. Taarifa zinasema kuwa, miripuko hiyo ya Damascus imefanywa na genge la kigaidi la Daesh (ISIS). Miripuko hiyo inaonesha mfungamano wa karibu mno uliopo baina ya magaidi wa Daesh na utawala pandikizi wa Israel na imetokea ili kuusaidia utawala wa Kizayuni ambao hivi sasa umekwama kwenye kinamasi cha maandamano, migogomo na migogoro ya ndani. Tatu: Wahanga wa miripuko hiyo ya Damascus ni raia wa kawaida hasa wanawake na watoto wadogo. Mwanamke mmoja ameuawa shahidi na wanawe watatu wamejeruhiwa kwenye miripuko hiyo ya kigaidi. Huu ni ushahidi wa kutosha kuwa magaidi hao na mabwana wazo Wazayuni na Wamagharibi, hawana chembe ya huruma na hawajali nani atakuwa muhanga katika hujuma zao za kiwoga na za kigaidi. Nne: Miripuko ya kigaidi ya mjini Damascua Syria na kuuawa shahidi na kujeruhiwa raia na watu wa kawaida kumenyamaziwa kimya na jamii ya kimataifa. Kama jamii hiyo inayojidai ni ya kimataifa isingelikuwa ni muungaji mkono wa vitendo vya kigaidi na vita dhidi ya dini, bila ya shaka yoyote ingeacha kuyaunga mkono magenge ya kigaidi ili jinai hizo zisijirudie tena. Lakini ndio kwanza tunayaona madola ya Magharibi na Kizayuni yamesimama kidete kuendeleza chuki dhidi ya dini ya Kiislamu na kudhalilisha mafundisho ya dini kiujumla. Tano: Miripuko ya mabaomu kwenye Haram ya Bibi Zainab SA katika viunga vya mji mkuu wa Syria, Damascus na kwenye maeneo mengine ya nchi hiyo ya Kiarabu, imetokea katika mazingira ambayo nchi hiyo iko chini ya mashinikizo na vikwazo vikubwa vya Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya licha ya madola hayo ya Magharibi kudai kuwa eti yanawajali raia. Inaonekana ni kwa kuzingatia nukta hizo tano ndio maana Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan'ani sambamba na kutoa mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Syria na hasa familia za wahanga wa miripuko hiyo ya Damascus, akakumbusha kwamba, wakati huu ambapo wananchi wasio na hatia wa wako chini ya mashinikizo ya kidhalimu ya Marekani na baadhi ya madola ya Magharibi, wanashambuliwa pia na magaidi na utawala wa Kizayuni huku jamii ya kimataifa ikiendelea kukaa kimya kana kwamba wananchi hao wa Syria si wanadamu.
342/